Jumapili 28 Desemba 2025 - 22:00
Kiongozi mwandamizi wa Hizbullah: Muqawama hautapambana na jeshi na hautaruhusu fitina ya ndani

Hawza/ Sheikh Ali Damoush amesema: hapo awali ilielezwa kwamba kukamilishwa kwa hatua za jeshi kusini mwa Mto Litani kulitegemea kusitishwa kwa mashambulizi na kujiondoa kwa adui “Muisraeli” kutoka kstika maeneo aliyoyakalia.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ali Damoush, Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah, katika khutba ya Swala ya Ijumaa aliyotoa katika mujtamaa wa Sayyida Zaynab (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) katika eneo la “Bir al-Abd”, alisema: hapo awali ilibainishwa kwamba kukamilika kwa hatua za jeshi kusini mwa Litani kulitegemea kusitishwa kwa mashambulizi na kujiondoa adui “Muisraeli” kutoka katika maeneo aliyoyakalia.

Aliongeza kusema: hata hivyo, ukweli ni kwamba mpango huu ulishindwa kadiri siku zilivyopita; kwa sababu jeshi limekamilisha hatua zake na linakaribia kumaliza kile kinachoitwa “awamu ya kwanza”, ilhali mashambulizi hayajasitishwa wala kujiondoa hakujatekelezwa. Kinyume chake, adui “Muisraeli” ameongeza mashambulizi yake na hajachukulia umuhimu wowote kwa hatua za jeshi.

Sheikh Damoush alisisitiza kuwa; mojawapo ya makosa makubwa ya serikali ya Lebanon ilikuwa ni kutenganisha utekelezaji wa hatua zake, kwa mujibu wa makubaliano, na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na adui “Muisraeli”; jambo lililoiweka Lebanon katika nafasi ya nchi inayotekeleza makubaliano ya upande mmoja tu.

Alibainisha kuwa; hatua zilizomo katika makubaliano kusini mwa Litani ni wajibu wa pande zote mbili, si upande mmoja pekee; na iwapo Lebanon imetimiza wajibu wake, basi ni lazima pia adui “Muisraeli” atekeleze ahadi zake.

Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah alisema: kile kinachoitwa “awamu ya kwanza” hakitakamilika isipokuwa baada ya adui kutekeleza ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano, yaani kujiondoa katika maeneo aliyo yakalia, kusitisha mashambulizi, kurejea kwa wakazi na kuanza ujenzi upya. Ukuu wa nchi haupatikani kwa kuondolewa jeshi la Lebanon pekee; ili hali adui “Muisraeli” anaendelea na uvamizi, mashambulizi na ukiukaji wa mamlaka ya Lebanon ardhini, baharini na angani.

Alisisitiza kuwa; mfululizo wa kutoa misamaha na mapendeleo bado unaendelea hadi leo, licha ya kuendelea mashambulizi na dharau ya adui “Muisraeli” na Marekani dhidi ya hatua na mapendekezo yaliyotolewa na serikali. Wakati huo huo, wapo watu ambao hata chini ya mashambulizi ya “Israel” wanataka kuhamia kaskazini mwa Litani, bila kuwepo juhudi yoyote ya kweli ya kusitisha mashambulizi au kulazimisha kujiondoa.

Sheikh Damoush alieleza kuwa; ingekuwa bora zaidi kwa wale wanaotaka kuhamia “awamu ya pili” kudai utekelezaji wa ahadi za adui, badala ya kuendana na matakwa yake, na badala ya kukubali maagizo ya Marekani ya kutoa mapendekezo ya bure, wangeliweka shinikizo kwa Marekani ili mashambulizi yakomeshwe.

Aliongeza kuwa; Marekani ina uwezo wa kusitisha mashambulizi na kumlazimisha adui kuondoka, kwa sababu mashambulizi ya “Muisraeli” yanafanyika kwa mshikamano na muingiliano kamili kati ya Marekani na “Israel”. Marekani ni mshirika kamili katika vitisho na mashambulizi yote ambayo adui “Muisraeli” huyafanya kila siku dhidi ya Lebanon.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hizbullah aliendelea kusema: yote yanayotokea leo—iwe katika kiwango cha mashambulizi na mauaji ya kisiasa, au katika kiwango cha mashinikizo ya kisiasa, mzingiro, vikwazo vya kiuchumi na kifedha, pamoja na uchochezi kutoka kwa mawakala wa ndani—yote haya yanalenga kuiingiza Lebanon na jeshi lake katika fitina, kuvichochea dhidi ya Muqawama, na kuilazimisha Hizbullah kurudi nyuma au kujisalimisha.

Sheikh Damoush aliongeza: Marekani, “Israel” na mawakala wa ndani wanatumia zana zote kufanikisha malengo haya, lakini wanapaswa kujua kwamba Muqawama hautapambana na jeshi, hautaruhusu fitina ya ndani, na hautarudi nyuma wala kujisalimisha; wanapaswa kukata tamaa.

Kuweka matumaini katika kuisukuma serikali, jeshi na jamii inayounga mkono Muqawama kukabiliana na Muqawama ni kamari iliyoshindwa, na kila siku inazidi kuthibitishwa kuwa inaelekea kwenye kushindwa zaidi.

Sheikh Damoush aliendelea kusema: sisi ndani ya Hizbullah tumejikita katika haki yetu, ili mradi tu kuna uvamizi na ukaliaji. Yeyote anayefikiri anaweza kuupindisha mkono wa Muqawama, amekosea vibaya. Hakuna kitu kitakachotulazimisha kuachana na haki hii; si mashambulizi, si mauaji ya kulenga watu, si mzingiro, si vikwazo, si kampeni za vyombo vya habari, wala chuki tunazozisikia kutoka kila upande.

Mwisho wa hotuba yake alisema: watu wetu waaminifu wako pamoja nasi na wako upande wetu. Wanaonesha uaminifu wao kutokana na amana ya mashahidi kupitia uwepo wao uwanjani na kushikamana kwao na Muqawama, licha ya maumivu yote, mateso, sera za mashambulizi na mashinikizo ambayo maadui hutumia kuwashawishi waachane na Muqawama. Mashambulizi endelevu ya adui “Muisraeli”, serikali ya Marekani na mawakala wao wa ndani hayataweza kubadilisha imani za watu wetu wala msimamo wao kuhusu Muqawama; bali yataongeza zaidi azma ya Muqawama kuendelea katika njia hii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha